Zaidi ya watu 30,000 waathiriwa na kimbunga Madagascar
23 Februari 2022Zaidi ya watu 30,000 walihamishiwa kwenye makazi salama hapo awali kabla ya kimbunga hicho kuwasili, ofisi ya taifa inayoshughulika na maafa nchini Madagasca inakadiria zaidi ya watu 250,000 wanaweza kuathiriwa na kimbunga hicho cha hivi karibuni.
Hadi sasa hakuna ripoti ya vifo wala majeruhi kutokana na kimbunga Emnati, mamlaka nchini humo inasubiri kupita kwa kimbunga hicho.
Hata hivyo viongozi wa eneo hilo na mashuhuda wanaripoti uharibifu mkubwa wa nyumba na majengo mengine katika eneo hilo la kusini Mashariki.
Soma zaidi:Kimbunga Batsirai chasababisha vifo vya watu sita Madagascar
Madagascar, kisiwa kilicho karibu na pwani ya mashariki ya Afrika kinachojulikana kwa wanyamapori na hazina ya asili isiyoharibika, sasa imepigwa na dhoruba nne kuu za kitropiki katika mwezi uliopita na vifo kuripotiwa huku uhaba wa chakula ukishuhudiwa.
Kulingana na shirika la mpango wa chakula la umoja wa mataifa takriban watu 400,000 wapo katika hatari ya kukabiliwa na njaa kutokana na hali ya ukame katika eneo la kusini mwa nchi hiyo mwaka uliopita.
Mamlaka zaonya hatari zaidi
Shirika la hali ya hewa la umoja wa mataifa hapo awali lilionya juu ya vimbunga zaidi vya kitropiki vyenye athari kubwa ambavyo vinahusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kupiga zaidi katika eneo hilo.
Mamlaka ya hali ya hewa nchini humo imesema Emnati kilitua karibu usiku wa manane kwa saa za huko katika wilaya ya Manakara Atsimo katika kusini-mashariki, na upepo wa wastani wa 135 kph (84 mph) na upepo mkali kama 190 kph (118 mph).
Mikoa sita ya kusini mashariki ambayo ilishambuliwa na kimbunga Batsirai tayari imekwishapewa tahadhari.Mawasiliano ya simu yalitatizika na maeneo yote yalisalia gizani tangu mapema wiki hii.
Soma zaidi:Wananchi wa Kusini mwa Madagascar wakaribia kutumbukia kwenye baa kubwa la njaa
Mkazi wa Manakara, Gabriel Filiastre amesema familia yake iliungana na wengine kupata hifadhi ndani ya ukumbi mkuu wa hoteli anakofanyia kazi ameongeza kimbunga hicho kimefanya uharibufu mkubwa kuliko hata kile cha awali,nyumba zao zimejaa maji hivyo hawawezi kulala.
Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yameonya juu ya uhaba mkubwa wa chakula, kutokana na mazao kuharibiwa.
Hapo awali taarifa za mifumo ya hali ya hewa ilionesha kuwepo kwa vimbunga 8 hadi 12 katika eneo hilo Madagascar.