Zelenskiy ahutubia Baraza la Usalama, ataka Urusi iadhibiwe
6 Aprili 2022Mzozo wa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umejadiliwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo Rais Volodomyr Zelenskiyalilihutubia kwa njia ya video.
Zelenskiy aliuliza ikiwa kuna haja ya kuwepo kwa baraza la usalama, ambalo amesema lilishindwa kufanya chochote baada ya Ukraine kuvamiwa na Urusi tarehe 24 Februari, kwa vile Urusi inayo kura ya turufu katika baraza hilo, kama ilivyo kwa Marekani, Uingereza, Ufaransa na China.
Urusi imekuwa ikikabiliwa na shutuma na shinikizo kali kutoka nchi za magharibi, baada ya kugundulika makaburi ya watu wengi katika mji wa Bucha ulio kaskazini mwa Ukraine, ambao hadi siku chache zilizopita ulikuwa ukidhibitiwa na vikosi vya Urusi.
Afisa wa serikali ya Ukraine anayesimamia haki, Lyudmyla Denisova amesema kati ya maiti 150 na 300 zimefukiwa katika kaburi moja.
Ni uzushi wa nchi za magharibi: Urusi
Urusi hata hivyo imeendelea kuzikanusha tuhuma hizo. Balozi wake katika Umoja wa Mataifa Vassily Benenzia, akizungumza baada ya rais Zelenskiy, amesema na hapa nanukuu, ''kwa mara nyingine tumesikiliza uongo chungu nzima kuhusu jeshi la Urusi na askari wake.'' Mwisho wa kumnukuu.
Soma zaidi: Ukraine yailaumu Urusi kwa uhalifu wa kivita
Balozi huyo ameongeza kuwa simulizi za mauaji ya mjini Bucha ni uongo uliotungwa na nchi za magharibi, lengo likiwa kuiaibisha Urusi.
Lakini nchi za magharibi hazikuishia tu katika kuishutumu Urusi, bali zimepiga hatua na kutafakari vikwazo zaidi vya kuiwekea nchi hiyo. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni kupiga marufuku uagizaji wa makaa ya mawe kutoka Urusi, ambao una thamani ya karibu dola bilioni 10, na kusimamisha mauzo ya bidhaa kutoka Ulaya kwenda Urusi, pia yenye thamani ya dola karibu bilioni 11.
Urusi yatengwa kidiplomasia, yasema hatua hiyo haina tija
Marufuku hizo ni nyongeza kwa hatua nyingine za kidiplomasia, ambapo nchi saba za Umoja wa Ulaya zimewafungisha virago wafanyakazi wa balozi za Urusi wapatao 150 katika muda wa siku mbili.
Lakini licha ya vikwazo hivyo ambavyo nchi za magharibi hazijawahi kuiwekea nchi yoyote nyingine, Ukraine imesema havitoshi, na inataka Ulaya kuvunja uhusiano wowote wa kibiashara na Urusi, licha ya rais wa Ukraine, kusema mwenyewe hana chaguo jingine ila kuzungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin kama njia pekee ya kumaliza vita.
Soma zaidi: Ujerumani, Ufaransa kufukuza dazeni za wanadiplomasia wa Urusi
Urusi imesema imesikitishwa na kufukuzwa kwa wanadiplomasia wake, na msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov amesema hatua hiyo ni kutotazama mbali, kwa sababu inafunga mlango wa mazungumzo ambayo ni muhimu kumaliza uhasama na kuelekea maridhiano.
Afisa huyo ameongeza kuwa Urusi italazimika kuzijibu hatua hizo.
Na kwenye uwanja wa mapigano, Ukraine imesema makombora ya jeshi la majini la Urusi yameipiga meli yenye usajiri wa kigeni karibu na mji uliozingirwa wa Mariupol, na meya wa mji huo Vadym Boichenko ameliambia shirika la habari la afpe kuwa hali ya kibinadamu ni mbaya kuliko inavyoweza kufikirika.
-afpe, rtre