Ziara ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani nchini Uturuki
19 Oktoba 2010Ziara ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Christian Wulff nchini Uturuki,na mjadala unaoendelea kuhusu wageni nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Tuanze lakini na ziara ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,Christian Wulff nchini Uturuki.Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung linaandika:
Ingawa Wulff amekwenda Uturuki akiwa rais wa shirikisho,hata hivyo hatokosa la kusema kuhusiana na kiu cha serikali ya Erdogan cha kujiunga na Umoja wa Ulaya.Hata hivyo dini itashikilia nafasi muhimu wakati wa ziara hiyo ya siku nne ya rais wa shirikisho.Na hapo ndipo changamoto kubwa zinapokutikana.Kwa upande mmoja kwasababu serikali ya Uturuki,kupitia idara zake zinazoshughulikia masuala ya dini,inataka kuendeleza ushawishi wake kwa kutuma maimam nchini Ujerumani.Kwa upande mwengine changamoto hizo zinahusiana na nafasi ya jamii ndogo ya wakristo nchini Uturuki,Masuala ya kiuchumi,ambayo kawaida hugubika ziara kama hizi,safari hii yamewekwa nyuma.
Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika:
Hakuna chochote kitakachosaidia kuhimiza mjadala kuhusu hali ya siku za mbele si onyo la tahadhari la Trittin,si matamshi ya Seehofer yanayowapanulia uwanja wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wala si hotuba mfano wa ile ya Angela Merkel kuhusu kushindwa utaratibu wa kuishi pamoja watu wa tamaduni tofauti.Akiwa ziarani nchini Uturuki kwa hivyo Wulff atafanya kila liwezekanalo kuganga yajayo.Sio kutenganisha bali kuunganisha.Atatilia mkazo nafasi ya kufanikiwa juhudi za nchi zote mbili kwaajili ya kuishi pamoja jamii zenye tamaduni na mila tofauti.Bila ya kuficha mafanikio yaliyopatikana na bila ya kutia chunvi walakini uliopo.
Mada ya kujumuishwa wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii imehanikiza tangu wiki kadhaa sasa humu nchini.Waziri wa elimu Anette Schavan amependekeza shahada za wahamiaji wanaoishi humu nchini zitambuliwe rasmi.Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika:
Si haba.Hata kama limekawia lakini limetolewa.Vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP wanataka kuwasilisha mswaada wa sheria kuhusu wasomi wenye asili ya kigeni.Fikra ni nzuri hata kama imekawia kutolewa.Kwa miaka sasa imekua ikijulikana kwamba makampuni yanakosa wataalam vijana.Ujerumani inakabiliana na kizungumkuti-idadi ya wazee inaongezeka na hali hiyo haitobadilika hata kama idadi ya wanaozaliwa itaongezeka.Ikiwa Ujerumani haitotaka kupoteza sifa zake kama mojawapo ya taifa muhimu kiuchumi,basi haitakuwa na budi isipokua kuandaa mkakati madhubuti kuhusu wahamiaji na kudhaminiwa na vyama vingi vya kisiasa kwa namna ambayo utapelekea kufanikiwa juhudi za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii.
Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/Inlandspresse/dpa
Mpitiaji:Abdul Rahman