Hotuba ya Krismasi: Rais wa Ujerumani atoa wito wa umoja
24 Desemba 2024Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika hotuba yake ya Krismasi mwaka huu wa 2024 ametoa wito wa umoja kwa kuzingatia matukio ya hivi majuzi nchini humo.
Steinmeier alianza hotuba yake kwa kuzungumza juu ya shambulio baya katika soko la Krismasi katika mji wa Magdeburg, mashariki mwa Ujerumani.
"Kivuli cheusi kimetanda kwenye Krismasi hii," alisema, akiongeza kusema "tunaweza kuwaza na kufikiria tu" kile ambacho ndugu na jamaa za wahasiriwa wanachopitia baada ya kuwapoteza wapendwa wao.
Rais wa Ujerumani aliwaambia wote waliofikwa na misiba au jamaa zao kujeruhiwa kwamba hawako peke yao katika maumivu yao bali watu nchini kote wanawahurumia na wanaomboleza pamoja nao. Rais Steinmeier, pia amewashukuru polisi na wahudumu wa afya kwa kazi yao baada ya kutokea shambulio hilo.
Soma Zaidi: Idadi ya waliojeruhiwa kwenye mkasa wa Magdeburg yaongezaka
Akizungumzia athari za shambulio hilo kwa jamii, Steinmeier ametoa wito kwa watu nchini Ujerumani kukataa kugawanywa.
Amesema "Chuki na vurugu zisiwe hatma au neno la mwisho kwetu". Rais wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier amewasisitizia watu wa Ujerumani kwamba wakatae kabisa kutenganishwa na badala yake wasimame pamoja!
Mitazamo ya kisiasa nchini Ujerumani imekuwa 'mibaya'
Mbali na kutaja vita vinavyoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Rais Steinmeier pia alizungumzia uchaguzi ujao wa Ujerumani, utakaofanyika Februari 2025.
Kiongozi huyo wa Ujerumani amesema "Kuna kiasi kikubwa cha kutoridhika kuhusu siasa, biashara, kuhusu ukosefu wa haki," amesema kihitimisha kwamba mitazamo ya hayo yote katika nchi ya Ujerumani imekuwa mibaya ambapo wakati mwingine inachochea chuki, katika maisha ya watu ya kila siku.
Soma Zaidi: Shambulio la Magdeburg lachukua mkondo mpya wa kisiasa
Licha ya changamoto hizo, Rais wa Ujerumani amesema anaamini katika demokrasia ya nchi hiyo na Sheria yake ya Msingi, au katiba ambayo imekuwa madarakani tangu mwaka 1949.
Rais Steinmeier amesisitiza kwamba licha ya changamoto nyingi kuwepo lakini ni lazima wajerumani wakabiliane nazo. Amesema ni lazima watu wazungumze kwa uwazi kuhusu kile kinachoendelea na kuhusu kile kinachohitajika kufanywa haraka.
Rais wa Ujerumani pia amevizungumzia vita vya Ukraine, Mashariki ya Kati na katika maeneo mengine duniani, amesema anaamini kwamba njia mpya zitafunguka kwa haya yote katika siku zijazo.
Rais wa Ujerumani pia ametuma ujumbe kwa vijana wa nchi hiyo.
"Mnahitajika, tena sana, katika maeneo mengi," alisema Rais wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier, akiongeza kuwa vijana wa Ujerumani "wanaweza na wanatakiwa wajenge njia na mustakabali wa Maisha yao ya siku zijazo.
Rais wa Ujerumani Frank Walter-Steimeier amesema anatambua kwamba kuna hali ya kutoridhika sana kuhusu siasa nchini Ujerumani lakini amesisitiza kwamba demokrasia ya nchi hiyo iko imara.
Amesema kuanguka serikali ya Ujerumani sio mwisho wa dunia.
Mnamo Desemba 27, Rais Frank-Walter Steinmeier anatarajiwa kuitisha uchaguzi mpya ambayo kulingana na mipango ya sasa tarehe iliyopangwa ya kufanyika uchaguzi huo ni Februari, 23, 2025.
Vyanzo: DPA/AFP/ /dw/en/german-president-steinmeier-calls-for-unity-in-christmas-address/a-71149141