1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiBurkina Faso

HRW: Makundi yenye itikadi kali yanawaua raia Burkina Faso

18 Septemba 2024

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limesema Jumatano kuwa katika miezi ya hivi karibuni, wapiganaji wenye itikadi kali wameongeza mashambulizi yao dhidi ya raia nchini Burkina Faso.

https://p.dw.com/p/4klhM
Nembo ya Shirika la Human Right Watch
Nembo ya Shirika la Human Right WatchPicha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Tangu Februari mwaka 2024, HRW imesema kwamba  wapiganaji wa  itikadi kali  wamefanya mashambulizi saba, ambayo yaliua takriban raia 128 na kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

Ilaria Allegrozzi, mtafiti mwandamizi wa shirika hilo katika kanda ya Sahel amesema kunashuhudiwa ongezeko la ghasia na mauaji vinavyoendeshwa na makundi yenye itikadi kali  nchini  Burkina Faso  na kwamba huo ni unyanyasaji wa kikatili kwa maadili ya binadamu.

Katika ripoti iliyojaa ushuhuda, HRW ilijumuisha baadhi ya matukio ya kikatili ikiwa ni pamoja na mauaji ya nyumba kwa nyumba, ukatili wa uchinjaji, kukatwa kwa miili na ubakaji wa wanawake. Shambulio la mwezi Februari dhidi ya waumini wa kanisa huko Essakane lilisababisha vifo vya watu 12 waliouawa kikatili.

Raia wa Burkina Faso wakitoka Barsalogho hadi Kaya
Raia wa Burkina Faso wakitoka Barsalogho hadi KayaPicha: Olympia de Maismont/AFP

Ukinukuliwa katika ripoti hiyo, Mradi wa kukusanya data katika maeneo ya migogoro (ACLED) imeorodhesha zaidi ya watu 26,000 waliouawa nchini Burkina Faso wakiwemo wanajeshi, wanamgambo na raia tangu kuanza kwa vita mnamo mwaka 2016.

Soma pia: Zaidi ya watu 10 wameuawa katika shambulio Burkina Faso

Katika miezi minane ya kwanza ya mwaka huu, ACLED ilirekodi vifo zaidi ya 6,000, ikiwa ni pamoja na karibu raia 1,000 waliouawa na makundi yenye itikadi kali. HRW imesema takwimu hizo hazikujumuisha raia 100 hadi 400 waliouawa katika shambulio la Agosti 24 huko Barsalogho, katikati mwa nchi hiyo.

Raia "walazimishwa" kurejea katika maeneo tete kiusalama

Mkazi wa huko Niamana, magharibi mwa Burkina Faso anasema wanakabiliwa na chaguo gumu. Kwa upande mmoja serikali inawataka kurejea katika vijiji vyao ambako bado hali ya usalama ni tete, na kwa upande mwingine, makundi ya itikadi kali yanawashambulia wanaporejea kwenye mashamba na nyumba zao.

Soma pia: HRW yahimiza uchunguzi juu ya matukio ya kinyama yaliofanywa na jeshi la Burkina Faso

Alipoulizwa na HRW kuhusu madai hayo ya kuwalazimisha raia kurejea kwenye makazi yao, waziri wa sheria wa nchi hiyo, Edasso Rodrigue Bayala, alisema kuwa hatua hiyo huchukuliwa kwa hiari na hutanguliwa na hatua za kuilinda mitaa na kufungua upya huduma za kimsingi za kijamii.

Mtawala wa kijeshi wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traore
Mtawala wa kijeshi wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traore Picha: Donat Sorokin/TASS/dpa/picture alliance

Kundi la Jama'at Nusrat al-Islam wal Muslimeen (JNIM) lenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda huendesha operesheni zake katika mikoa 11 kati ya 13 ya Burkina Faso. Kundi hilo pia mara kwa mara hufanya mashambulizi katika nchi jirani za Niger na Mali. Jana Jumanne, kundi hilo lilidai kuhusika na shambulizi katika mji  mkuu wa Mali- Bamako  dhidi ya uwanja wa ndege wa kijeshi na kambi ya mafunzo kwa maafisa wa polisi.

Ripoti ya HRW inaonyesha matatizo yanayoukabili utawala wa kijeshi wa Kapteni Ibrahim Traore katika kujaribu kuzuia ongezeko hili la ghasia za makundi ya itikadi kali nchini Burkina Faso. Traore aliponyakua madaraka katika mapinduzi ya Septemba mwaka 2022, kiongozi huyo wa jeshi aliahidi kurejesha udhibiti wa nchi hiyo katika muda wa miezi sita, na kusema kuwa vita dhidi ya ugaidi ndiyo kipaumbele chake.

(Chanzo: AFP)