1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Korea Kusini: Maafisa zaidi wapigwa marufuku ya kusafiri

10 Desemba 2024

Mamlaka ya Korea Kusini imewapiga marufuku ya kusafiri maafisa wengine wakuu. Wakati huo huo Bunge limepitisha muswada wa kukamatwa mara moja, Rais wa Korea Kusini na baadhi ya maafisa wakuu kwenye serikali yake.

https://p.dw.com/p/4nyPU
Südkorea I Präsident Yoon Suk Yeol spricht im Präsidialamt in Seoul
Picha: South Korean Presidential Office/Yonhap/AP/picture alliance

Mamlaka nchini Korea Kusini imechukua hatua hiyo siku moja baada ya kumpiga marufuku ya kusafiri Rais Yoon Suk Yeol. Kwak Jong-geun, kamanda wa kikosi maalum cha jeshi ameiambia kamati ya bunge kuwa nchi inakabiliwa na wasiwasi kutokana na ofisi ya Rais kupungukiwa nguvu na kwamba hakuna msimamo rasmi kuhusu nani anayeongoza nchi?

Rais Yoon Suk Yeol, kwa sasa anakabiliwa na uchunguzi wa makosa ya jinai na uasi. Ameomba radhi kwa hatua yake ya kutangaza sheria ya kijeshi lakini wakati huo huo amesema hakubaliani na miito inayoongezeka ya kumataka aachie ngazi inayoolewa hata na baadhi ya wanachama wa chama chake.

Korea Kusini | Bunge la Taifa
Wabunge katika Bunge la Taifa la Korea KusiniPicha: Kim Hong-Ji/REUTERS

Kiongozi huyo wa Korea Kusini amesema amekabidhi hatma ya kisheria na kisiasa mikononi mwa Chama chake kinachotawala cha (PPP).  Chama hicho kimesema hii leo kwamba kinajadili juu ya mkakati wa kujiuzulu kiongozi huyo mnamo mwezi Februari au Machi kabla ya uchaguzi mpya nchini Korea Kusini unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili au Mei mwakani kuepusha hoja mpya ya upinzani inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni siku ya Jumamosi ya kumtaka Rais wa Korea Kusini aondolewe madarakani.

Soma Pia: Rais wa Korea Kusini Yoon anusurika kung'olewa madarakani

Wakati huo huo Bunge la Korea Kusini leo Jumanne limepitisha hoja ya kumteua mwanasheria maalum kumchunguza Rais Yoon Suk Yeol na maafisa wakuu wa serikali kuhusiana na kutangazwa sheria ya kijeshi nchini humo mapema mwezi huu. Hoja hiyo iliyowasilishwa na chama kikuu cha upinzani, cha Democratic Party, imepitishwa kwa kura 210 dhidi ya kura 63 huku wajumbe 14 wakiamua kutoshiriki kwenye zoezi hilo.

Wabunge pia wamepitisha mswada wa kutaka kukamatwa mara moja kwa Rais Yoon na baadhi ya maafisa wa serikali kutokana na agizo la Rais la sheria ya kijeshi, ambalo ni la kwanza kutolewa nchini Korea Kusini katika kipindi cha zaidi ya miaka 40. Spika wa Bunge Woo Won Shik alitangaza matokeo hayo."Kati ya jumla ya kura 288, kura 191 zimeunga mkono, 94 zimepinga, wajumbe watatu wamejiepusha kupiga kura. Natangaza, kwamba mswada unaohimiza kukamatwa mara moja wale wote wanaokabiliwa na mashtaka ya uasi, umepitishwa."

Korea Kusini
Katikati mbele Kiongozi wa chama cha upinzani cha Demokratic nchini Korea Kusini Lee Jae-myungPicha: YONHAP/REUTERS

Idadi ya watu watakaokamatwa imebadilishwa kutoka watu saba hadi watu wanane kwa kumwongeza Rais Yoon Suk Yeol. Wizara ya Sheria imempiga marufuku Yoon na maafisa wengine wanane kuondoka nchini kwa vile mamlaka inawaona kama washukiwa wakuu katika kesi kuhusu kutangazwa kwa sheria ya kijeshi.

Ni mara ya kwanza kwa rais aliyeko madarakani nchini Korea Kusini kuwekewa marufuku ya kusafiri.

Wakati huo huo, Mahakama ya Kati ya mjini Seoul imesema inalipitia ombi la waendesha mashtaka la kutaka kibali cha kumkamata aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Kim Yong Hyun, ambaye anatuhumiwa kwa kupendekeza sheria ya kijeshi kwa Rais Yoon na kuwapeleka wanajeshi katika Bunge la Taifa kwa ajili ya kuwazuia wabunge hao wasiipigie kura. Kim amezuiliwa tangu Jumapili. Ikiwa hati ya kukamatwa itatolewa, atakuwa mtu wa kwanza kukamatwa katika kesi hiyo.

Korea Kusini| Seoul | Maandamano
Mamia ya watu wafanya maandamano nje ya Bunge la Taifa la Korea KusiniPicha: Chris Jung/NurPhoto/picture alliance

Mamia ya watu wamefanya maandamano hii leo Jumanne jioni nje ya Bunge la Taifa, wakipunga vibendera na wengine wakiwa wameshikilia mabango yaliyoandikwa, "Yoon Suk Yeol ashitakiwe, ni mhalifu aliyongoza uasi."

Soma Pia: Rais wa Korea Kusini aomba radhi kwa taifa

Chama cha PPP kimesema kuwa Yoon, aliye na umri wa miaka 63, amekubali kukabidhi madaraka kwa waziri mkuu na mkuu wa chama hicho, lakini upinzani unapinga na umesema hayo ni mapinduzi ya pili.

Vyanzo: AFP/AP