Netanyahu aanza ziara nchini Marekani
22 Julai 2024Netanyahu aliitaja ziara hiyo kuwa ni "safari muhimu sana" ambayo inakuja wakati wa "mashaka makubwa ya kisiasa", akimaanisha uamuzi wa Rais wa Marekani Joe Biden kutogombea tena urais katika uchaguzi wa mwezi Novemba na wakati huu ambao utawala mjini Washington ukiishinikiza Israel kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano na kundi la Hamas.
Siku ya Jumatano, waziri mkuu huyo wa Israel aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi atakuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kuhutubia mara nne mkutano wa pamoja wa mabaraza hayo mawili ya Bunge, akivunja rekodi ya aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Winston Churchill.
Netanyahu anayetarajiwa pia kukutana na Biden ambaye atasalia kuwa rais wa Marekani hadi Januari 20 mwaka ujao, amesema kuwa katika hotuba yake kwa Baraza la Congress, atatafuta uungwaji mkono wa pande mbili ambao amesema ni muhimu mno kwa Israel, na kwamba bila kujali watu wa Marekani watamchagua nani kuwa rais ajaye, Israel inasalia kuwa mshirika muhimu wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani
Washington inahofia ukosoaji kutokana na ongezeko la vifo vya raia katika Ukanda wa Gaza, huku Netanyahu akiwekwa tumbo joto na maandamano ya familia za mateka waliochukuliwa na Hamas. Uongozi wa Biden na baadhi ya mawaziri wa Israel wanasema makubaliano yaliyojadiliwa kwa msaada wa wapatanishi kutoka Qatar, Misri na Marekani yanawezekana.
Lakini waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akisisitiza kuwa njia pekee ya kulitokomeza kundi la Hamas na kuwakomboa mateka waliosalia ni kuendeleza vita na kuongeza kasi ya mashambulizi.
Mzozo wa Gaza unatishia kutanuka zaidi
Siku ya Jumatatu, mapigano makali yameendelea kuripotiwa huko Gaza hasa eneo la kusini katika mji wa Rafah. Jeshi la Israel limewataka Wapalestina kuyahama maeneo yaliyotajwa hapo awali kuwa "salama". Watu 15 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa kufuatia shambulio la Israel, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka ya afya inayodhibitiwa na Hamas.
Soma pia:Koopsman: Nitaendela kushinikiza suluhu ya mataifa mawili
Mzozo huu wa Gaza unatishia pia kutanuka hadi Lebanon ambapo Israel inaendelea kukabiliana na wanamgambo wa Hezbollah lakini pia ikipambana na waasi wa Kihouthi kutoka Yemen ambao wamedai kuyashambulia siku ya Jumapili maeneo kadhaa ya kimkakati ya Israel baada ya ghala lao kushambuliwa katika mji wa bandari wa Hodeidah . Yaser al Dourani ni mkaazi wa Sanaa, mji mkuu wa Yemen:
"Hata watushambulie kiasi gani, daima tutaunga mkono hoja ya Wapalestina. Hatutoyumba, hatutarudi nyuma hata watushambulie kiasi gani, hata waharibu kiasi gani. Kuanzia kwa myemeni mdogo hadi mkubwa, hatutoyumbishwa."
Wizara ya afya ya Yemen imesema shambulio hilo la Israel limesababisha vifo vya watu sita na kuwajeruhi wengine 83.
(Vyanzo: AP, DPAE, AFP, RTRE)