Urusi yaendeleza uvamizi Ukraine katika "siku ya giza" Ulaya
24 Februari 2022Ripoti za hivi punde zinaeleza kuwa wanajeshi wa Urusi wamevamia maeneo ya kusini, kaskazini na mashariki mwa Ukraine, na kuna taarifa za vifo katika kambi za kijeshi na miripuko karibu na miji kadhaa mikubwa nchini Ukraine.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imeiharibu miundombinu 74 ya kijeshi ya juu ya ardhi nchini Ukraine, vikiwemo viwanja 11 vidogo vya ndege, hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la RIA.
Soma pia: Maoni: Putin ametangaza vita
Polisi ya Ukraine imesema Urusi imefanya mashambulizi zaidi ya 200, naye naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine amesema baadhi ya Warusi wameshikwa mateka katika mapigano makali mashariki mwa Ukraine.
Wizara ya ulinzi mjini Kiev pia imethibitisha kuwa wanajeshi wake wapatao 40 wameuawa katika mashambulizi ya Urusi.
Mjini Kiev ving'ora vya tahadhari vimekuwa vikisikika, na watu wamejazana katika vituo vya treni wakijaribu kuuhama mji huo. Wengine wanatumia njia ya barabara ambapo msongamano mkubwa wa magari unashuhudiwa.
Soma pia:Putin atangaza operesheni za kijeshi Ukraine
Poland ambayo ni jirani wa Ukraine Upande wa magharibi, imeandaa treni za kuwasaidia wakimbizi kutoka Ukraine na kuweka vituo vya kuwapokea.
Pande mbali mbali zimelaani mashambulizi haya ya Urusi. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema leo ni siku ya giza kwa Ulaya kutokana na mashambulizi hayo, na kumuonya rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba amefanya kosa kubwa.
Janga barani Ulaya
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Putin ameamua kufuata njia ya damu kwa kuamuru mashambulizi dhidi ya Ukraine, ambayo Johnson ameyaita janga kwa bara Ulaya.
Tayari Marekani imepeleka iwanajeshi wapatao 800 katika ukanda wa Baltiki unaopakana na Urusi, wakiwa na ndege za kivita.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemtaka Rais Putin kuima nafasi amani, lakini katibu mkuu wa Umoja wa Kujihami wa NATO Jens Stoltenberg amesema wito huo wa Guterres hauna nafasi tena kwa sababu amani barani Ulaya imekwishavunjwa.
Soma pia: Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Ukraine
Mjini Washington, Rais Joe Biden anafanya mkutano wa dharura na washauri wake wa masuala ya usalama.
Stoltenberg ambaye jumuiya anayoiongoza ina ndege za kivita zipatazo 100 na manowari 120 zilizo tayari kwa vita, amesema yeyote asihadaike kwamba NATO haitahakikisha usalama wa wanachama wake. Ukraine sio mwanachama wa Jumuiya hiyo.
China kwa upande wake imesita kukiita kilichofanywa na Urusi kuwa ni uvamizi dhidi ya Ukraine, badala yake imezitaka pande zote katika mzozo huu kujizuia.
Hakuna juhudi kubwa za kidiplomasia zinazoendelea kwa wakati huu. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amezitaka nchi washirika kuvunja uhusiano wa kibalozi na Urusi, lakini Urusi imezionya nchi hiyo dhidi ya kuchukuwa hatua kama hiyo.
Chanzo: ape, rtre