1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Waziri Mkuu wa Haiti atangaza kujiuzulu

12 Machi 2024

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amekubali kujiuzulu pamoja na kuunga mkono juhudi za kikanda kuruhusu kipindi cha mpito kitakachowezesha uingiliaji kati wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/4dQIC
Waziri Mkuu wa Haiti  Ariel Henry
Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amekubali kujiuzulu, akisema uchaguzi unahitaji kufanywa haraka iwezekanavyo ili kuleta utulivu katika taifa hilo linalokabiliwa na ghasia za magenge.Picha: Andrew Kasuku/AP Photo/picture alliance

Tangazo la kujiuzulu kwake amelitoa wakati magenge ya watu wenye silaha yakiendelea kulitumbukiza taifa hilo la kanda ya karibia kwenye machafuko.

Mataifa ya Karibia yalifanikisha hatua ya kujiuzulu kwa Ariel Henry katika mkutano wa dharura uliofanyika Jamaica ambapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alitoa dola nyingine milioni 100 ili kufungua njia kwa kikosi cha usalama kitakachoongozwa na Kenya.

Soma pia:Jeshi la Marekani lapeleka vikosi kunusuru maafisa wake Haiti 

Henry amekubali kuondoka madarakani lakini anasubiri mkutano wa mjini Kingston utoe maelekezo kuhusu kipindi hicho cha mpito.

Katika hotuba ya kujiuzulu kwake aliyoichapisha kwenye mtandao, Henry amesema serikali anayoiongoza haiwezi kubaki katika hali ya kutojali na hakuna kujitolea kokote kunakoshinda taifa la Haiti.

"Kufuatia kikao cha Baraza la Mawaziri leo jioni, Serikali ninayoiongoza imekubali kuunda Baraza la Urais wa Mpito. Wajumbe wa Baraza hili watachaguliwa kwa makubaliano kati ya sekta mbalimbali za jamii nchini." Alisema Henry.

Kiongozi huyo aliendelea kusema "Haiti inahitaji amani, utulivu, na maendeleo endelevu. Haiti inahitaji kujenga upya taasisi zake za kidemokrasia." 

Rais wa Guyana Irfaan Ali ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya CARICOM, ametangaza kwamba Henry ataondoka mara tu mamlaka mpya ya mpito itakapowekwa.

Soma pia: Maelfu ya wanawake wajawazito Haiti hatarini kukosa huduma za afya

Rais Ali alimpongeza Henry, akisema "ametuhakikishia kwa matendo yake, kwa maneno yake, nia yake ya kujitolea."

Uongozi wa Mpito

Jumuiya ya CARICOM
Wakuu wa Jumuiya ya (CARICOM) wafanya mkutano mjini Kingston, Jamaica kujadili hali ya Haiti.Picha: Andrew Caballero-Reynolds via REUTERS

Maafisa wakuu kutoka Brazil, Canada, Ufaransa na Mexico walioshiriki mazungumzo hayo, katika taarifa na washirika wake na Umoja wa Mataifa, wamesema kuwa Baraza jipya la uongozi wa Mpito la Haiti litakaloundwa litakuwa na wapiga kura saba ambao watafanya maamuzi kwa wingi wa kura.

Saba hao watajumuisha wawakilishi wa vyama vikuu vya kisiasa, sekta ya kibinafsi na Montana Group, muungano wa mashirika ya kiraia ambao ulikuwa umependekeza serikali ya mpito mwaka wa 2021 baada ya mauaji ya Rais Jovenel Moise.

Vile vile jopo hilo litakuwa na viti viwili visivyopiga kura, kimoja cha mashirika ya kiraia na kingine cha kiongozi wa kanisa.

Vurugu za magenge

Vurugu za magenge Haiti
Mwanamume akipita matairi yanayoungua wakati wa maandamano ya kumtaka Waziri Mkuu Ariel Henry ajiuzulu.Picha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Magenge yamechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya nchi hiyo katika wiki za hivi karibuni na vurugu vimekuwa mbaya zaidi, miili imetapakaa mitaani, huku magenge yenye silaha yakipora watu na kuharibu miundombinu ya msingi.

Soma pia: Machafuko mabaya yaikumba Haiti

Viongozi wa magenge wamekuwa wakishinikiza kuondoka kwa Henry ambaye, alijitaja kama kiongozi atakayeleta mabadiliko, amesalia madarakani tangu 2021 wakati rais wa Haiti alipouawa. Haitihaijafanya uchaguzi tangu 2016.