Vita vya Gaza: Duru mpya ya mazungumzo kuanza mjini Doha
15 Agosti 2024Marekani, Misri na Qatar zinatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na wajumbe wa Israel mjini Doha katika duru hiyo mpya ya mazungumzo ambayo huenda ikawezesha kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita na hivyo kuleta matumaini ya kuepuka mzozo mpana zaidi wa kikanda.
Haikufahamika wazi ikiwa Hamas ingelishiriki mazungumzo hayo kwa kuwa wameituhumu Israel kuongeza masharti zaidi kwenye pendekezo la awali ambalo lilipendekezwa na Marekani na lililokuwa limekubaliwa na kundi hilo. Msemaji wa Hamas, Osama Hamdan ameliambia shirika la habari la AP kwamba kundi hilo linahitaji kujadili utekelezaji wa pendekezo lililotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden, na sio kuanzisha mazungumzo mapya.
Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani walizitolea wito Iran, Hamas na Israel kwamba hakuna upande wowote katika eneo hilo unaopaswa kuchukua hatua ambazo zinaweza kudhoofisha juhudi za kufikia makubaliano hayo.
Soma pia: Iran haitoishambulia Israel iwapo tu kutafikiwa usitishwaji mapigano Gaza
Ndugu za mateka wameandamana leo mjini Tel-Aviv wakiishinikiza serikali yao ya Israel kuafiki mpango huo. Zahiro Shahar Mor, ni mpwa wa mateka wa Israel Avraham Munder.
"Tunahitaji usitishaji mapigano ili kuwarejesha mateka wote. Hatuwezi kuiamini tena serikali ya Israel. Kwa muda wa miezi kumi iliyopita, imekuwa ikizuia juhudi zozote za kufikiwa makubaliano. Tunafahamu kuna mkutano wa kilele leo, tuna matumaini kidogo juu ya utayari wa wajumbe wa Israel kusaini makubaliano hayo. Na tunatoa wito kwa mataifa yote duniani, yatusaidie kuirekebisha hali hii."
Shinikizo na matumaini kwa mpango huo
Kusitishwa kwa mapigano huko Gaza kunaweza kusaidia kutuliza hali ya wasiwasi inayotanda katika eneo la Mashariki ya Kati . Wanadiplomasia wanatumai kuwa kufikiwa kwa makubaliano hayo kutaishawishi Iran na kundi la Hezbollah la Lebanon kuachana na dhamira yao ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kufuatia mauaji ya kamanda mkuu wa Hezbollah Fuad Shukur mjini Beirut na kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran.
Mpango huo wa awamu tatu ungelihusisha usitishwaji mapigano Gaza, kuachiliwa kwa mateka wa Israel pamoja na wafungwa wa Kipalestina. Wakati juhudi hizo za kimataifa zikiendelea, idadi ya vifo vya Wapalestina katika mzozo huu ambao umedumu kwa miezi kumi sasa, inakaribia kufikia watu 40,000, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka za afya huko Gaza zinazodhibitiwa na Hamas.
Soma pia: Amnesty: Israel ikomeshe mateso kwa Wapalestina Gaza
Katika hatua nyingine, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kulihutubia bunge la Uturuki katika mji mkuu Ankara leo Alhamisi, siku moja baada ya kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin mjini Moscow. Siku ya Jumatano, Abbas alikutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na kuzungumzia kuhusu vita vya Gaza na hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kufikia mpango wa kudumu wa usitishwaji mapigano.
Vyanzo: (AFP, AP, Reuters, DPAE)