1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarafu ya Uingereza yaanguka dhidi ya dola

Admin.WagnerD28 Septemba 2022

Sarafu ya pauni ya Uingereza imeshuka thamani kwa kiwango cha chini kabisa dhidi ya Dola ya Marekani baada ya waziri wa fedha wa nchi hiyo Kwasi Kwarteng kutangaza mpango kabambe wa punguzo la kodi.

https://p.dw.com/p/4HTl2
UK Liz Truss
Picha: House of Commons/AP Photo/picture alliance

Mpango huo unatajwa kuchochea wasiwasi kuhusu sera ya kiuchumi ya serikali wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na kitisho cha kutumbukia kwenye mdororo.

Benki Kuu ya England imelazimika kuingilia kati leo kwa kununua amana za serikali ili kuzuwia wawakezaji kupoteza imani kwa mwelekeo wa uchumi wa Uingereza.

Serikali ya waziri Mkuu Liz Truss Ijumaa ilizindua mpango wa punguzo la kodi wenye thamani ya pauni bilioni 45, katika juhudi za kuchochea ukuaji wa kiuchumi.

Lakini mpango huo hawakuambatana na punguzo la matumizi ya serikali au hata makadirio huru ya gharama, na kuibua waiwasi kwamba utasababisha kutanuka kwa deni la serikali na kuongezea mfumuko wa bei ambao tayari umefikia asilimia 9.9, karibu na kiwango cha juu kabisaa katika muda wa miaka 40.

Benk kuu yachukua hatua

Benki Kuu ya England imechukuwa hatua hii leo kuzuwia mporomoko wa dhamana za serikali uliosababishwa na hatua hiyo, ambayo pia imeshuhudia thamani ya sarafu ya pauni ikiporomoka kwa kasi dhidi ya dola ya Marekani, na kufikia kiwango cha chini kabisaa tangu 1972.

Uingiliaji wa dharura wa benki kuu unaamanisha kuwa benki hiyo itanunua dhamana na hatifungani za serikali kuanzia leo Jumatano hadi Oktoba 14 katika juhudi kutuliza masoko na kupunguza gharama za ukopaji wa serikali.

Soma zaidi:Truss afanya kikao chake cha kwanza na timu yake ya mawaziri

Jagjit Chadra, mkurugenzi wa taasisi ya taifa ya utafiti wa kiuchumi na kijamii, amesema moja ya mambo yanayofanya mzozo huo kuwa mgumu zaidi kutatua ni kwamba mpango uliotangazwa Ijumaa haukwenda sambamba na makadirio ya taasisi ya uwajibikaji wa kibajeti.

amesema mpango huo ulipaswa kutoa muelekeowa wazi juu ya urari wa deni la taifa ikilinganishwa na makusanyo ya ndani ya nchi hiyo kwa mwaka, kanuni ambayo ndiyo kiashiria cha ukubwa wa uchumi wa taifa hilo.

"Kutokuwepo chapisho sambamba na bajeti kulimaanisha kwamba watu wengi walikuwa wanabahatisha tu."

Alisema  Chadra na kuongeza kwamba hakukuwa na uhakika hasa nini ilikuwa maana ya hicho na anadhani hilo liliongeza kelele zilizoshudiwa wiki iliyopita.

Soma zaidi:Liz Truss ateuliwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza

Benki Kuu ya Uingereza imesema inaendelea kufuatilia kushuka kwa thamani ya pauni na haitasita kuongeza viwango vya riba ili kudhibiti mfumuko wa bei baada ya kufanya hivyo wiki iliyopita tu.

Serikali, IMF kuingilia kati mzozo huo

Wizara ya fedha ilisema itatangaza mpango wa kifedha wa muda wa kati Novemba 23, pamoja na makadirio ya kiuchumi ya ofisi ya uwajibikaji wa bajeti.

London | Kwasi Kwarteng Energieminister
Waziri wa fedha Uingereza Kwasi KwartengPicha: Justin Ng/Avalon/Photoshot/picture alliance

Hata hivyo uhakikisho huu haukusaidia kutuliza wasiwasi kuhusu sera za kiuchumi za serikali hiyo mpya.

Wakosoaji wamesema hatua zilizochukuliwa na waziri Kwarteng zitawanufaisha tu matajiri kuliko maskini, wakati ambapo mamilioni ya Waingereza wanateseka kutokana na mzozo wa gharama za maisha.

Katika uingiliaji usio wa kawaida, shirika la fedha la kimataifa IMF, lilisema jana jioni kwamba linafuatilia kwa karibu matukio hayo na kuisihi serikali mjini London kubadili mwelekeo, na kuonya kuwa hatua hizo za Uingereza zitachochea ongezeko la ukosefu wa usawa.

Katika bajeti yake waziri wa fedha Kwarteng alipunguza kiwango cha juu zaidi cha kodi ya mapato na kuondoa ukomo kwenye marupurupu ya watendaji wa benki.

Soma zaidi:Boris Johnson aaga, Truss kuwa waziri mkuu rasmi

Lakini pia alitangaza mpango wa kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi wote.

Waziri Mkuu mhafidhina Liz Truss alimteua Kwarteng kuchukua nafasi ya Rishi Sunak, aliemshinda katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya waziri mkuu na kushindwa na Truss.