Urusi inahujumu makubaliano ya Nyuklia ya Iran?
10 Machi 2022Licha ya kushuhudiwa kwa maendeleo katika mazungumzo ya kurejesha makubaliano ya nyuklia ya Iran ya 2015, mustakabali wa makubaliano hayo uko hatarini baada ya matakwa ya dakika za mwisho ya Urusi ya kufutiliwa mbali vikwazo ilivyowekewa na mataifa ya Magharibi.
Baada ya mazungumzo ya takriban miezi kumi na moja wapatanishi wanaonekana kukaribia kufikia mwafaka juu ya kufufua makubalianoya nyuklia ya Iran ya 2015, ambayo yaliondoa vikwazo kwa Tehran badala ya kuzuiwa kwa mpango wake wa nyuklia.
Soma zaidi:Mtambo wa nishati ya nyuklia washambuliwa Ukraine
Lakini mazungumzo yamekuwa magumu kutokana na hitaji la dakika za mwisho kutoka kwaUrusi la dhamana ya maandishi kutoka kwa Marekani kwamba vikwazo vingi vya Magharibi vinaivyolenga Moscow kutokana na uvamizi wake kwa Ukraine havitaathiri ushirikiano wake wa kiuchumi na kijeshi na Iran.
Marekani imelikataa ombi la Urusi huku Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken akisema kwamba matakwa hayo hayana msingi na vikwazo vya Urusi kutokana na uvamizi wake wa kijeshi Ukraine avihusiani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran.
Iran yasaka ufafanuzi kutoka Moscow
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Saeed Khatibzadeh aliwaambia waandishi wa khabari kwamba bado wanatafuta ufafanuzi kutoka Moscow kuhusu wanachohitaji kwenye madai yao.
Wakati huo huo mataifa Magharibi, yaliionya Moscow dhidi ya uvunjaji wa makubaliano hayo ambayo yanaelekea kukamilika katika kuzirejesha Marekani na Iran.
Katika taarifa ya pamoja ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa umoja wa Mataifa katika bodi ya ya magavana wa nchi 35 ya shirika la nyuklia walitoa wito kwa pande zote kufanya maamuzi muhimu ya kufunga mkataba na kwa Urusi kutoongeza masharti ya ziada.
Mtaalamu wa masuala ya Nyuklia katika Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama yenye makao yake mjini Berlin Hamidreza Azizi alisema,tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi huko Ukraine, kumekuwa na wasiwasi kwamba maendeleo mapya, haswa kuongezeka kwa makabiliano kati ya Urusi na Magharibi, yanaweza kuathiri vibaya makubaliano yalikufufuliwa makubaliano ya nyuklia ya Iran.
Soma zaidi:Iran yasema Marekani "inavuruga" mazungumzo ya nyuklia
Mtaalamu huyo ameiambia Dw kuwa kiini cha msingi wa wasiwasi ni kwamba Moscow inaweza kujaribu kuyachukua mazungumzo kwa manufaa yake au kuyatumia kama njia ya mazungumzo kufikia makubaliano na nchi za Magharibi kuhusu Ukraine.
Wanadiplomasia kutoka Iran na mataifa yenye nguvu duniani wamekuwa wakifanya mazungumzo mjini Vienna kwa miezi kadhaa kurejesha mkataba wa nyuklia wa 2015.
Washington inashiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kutokana na rais wa zamani Donald Trump kujiondoa kwenye makubaliano mnamo 2018.
Uvamizi wa kijeshi wa Urusi wazorozesha uchumi
Vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vimesababisha moscow kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na mataifa ya magharibi hatua ilisababisha uchumi wa Urusi Kudorora na kupanda kwa kasi bei ya bidhaa muhimu kama mafuta,gesi ngano na nyinginezo.
Iran inaweza kuuza nje mafuta zaidi na kufaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na kupanda kwa bei iwapo makubaliano ya nyuklia yatarejeshwa usafirishaji wa bidhaa ghafi, njia ya kiuchumi ya taifa hilo tajiri kwa mafuta, umedorora kutokana na vikwazo vya Marekani.
Soma zaidi:Umoja wa Ulaya waomba usalama wa nyuklia kuangaziwa
Makadirio yanaonyesha kuwa yalipungua kutoka takriban mapipa milioni 2.8 kwa siku mwaka wa 2018 hadi chini ya mapipa 700,000 kwa siku.
Mtaalamu wa masuala ya nishati Dalga Khatin Oglu anaamini kwamba hata kama vikwazo hivyo vitaondolewa, Iran haitaweza kurejesha nafasi yake sokoni mara moja kwa sababu wateja wake wakuu barani Asia ikiwemo Korea Kusini, Japan na India hawaagizi tena mafuta kutoka nje.